Thursday, October 28, 2010

31 Oktoba Jumapili ya 31 ya Mwaka C

31 Oktoba Jumapili ya 31 ya Mwaka C
Insha: Mungu Anayetafuta na Kuwaokoa Wenye Dhambi
Masomo: Hekima 11:22-12:1; 2 Thesalonika 1:11-2:22; Lk. 19:1-10

Jumapili iliyopita, masomo yalituonyesha umuhimu wa kuwa wanyenyekevu katika sala, na pia kumtegemea Bwana daima. Tulipewa mfano wa yule mtoza kodi aliyekwenda hekaluni kusali, naye akakaa kule numa kwa sababu hafai kamwe. Jumapili hii masomo yatufunulia Mungu mwenye huruma anayewatafuta na kuwaokoa wenye dhambi kwenye ile hadithi ya Zakayo. Somo la kwanza latuonyesha Mungu mwenye nguvu na mumbaji, lakini pia Mungu mwenye huruma, anayewatafuta na kuwasamehe wenye dhambi.

Hadhithi ya Zakayo mtoza kodi kwenye Injili, ambao ni Luka peke yake ameiandika, ni mfano wa kutuonyesha jinsi Mungu hututafuta ili kutuokoa. Tukumbuke kwamba Zakayo alikuwa mtoza kodi tajiri, aliyepata mali yake kwa rushwa kutoka Mayahudi wenzake. Hivyo watu walimchukia sana. Isitoshe, kulingana na amri za Kiyaudi, kila mtoza kodi alifikiriwa kuwa mwenye dhambi. Zakayo amesikia Yesu anapitia kule jijini la Jeriko, na akawa na hamu kubwa kumwona Yesu. Kumbe ile hamu ilikuwa neema ya Mungu, ikimwongonza hadi karibu na Yesu. Yesu pia alimtafuta na akamgusa Zakayo kiroho. Zakayo kwa ujasusi na hamu ameacha afisi na kaingia katika umati ambao ni mwingi. Kwa sababu ni mfupi, amepotea mle. Ndipo basi anakimbia mbele na kupotea tena. Mwishowe anapanda mti, ili amwone Yesu. Kwa kufanya hivyo anajitia katika hatari, kwa sababu wengi jijini wamjua kama “Mkurugezi wa Ushuru” wa serikali ya kikoloni ya Roma. Alipokaribia ule mti mahali Zakayo alikuwa amepanda, Yesu alimwita: "Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani mwako". Yesu alienda kwa Zakayo "kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa kilichopotea". Kwenye ile karamu aliyemtengenezea Yesu, Zakayo aligeuka moyoni kabisa akawa mtu mpya. Akabadilika kiroho na maishani mwake kabisa. Hata Yesu mwenyewe alihakikisha kwamba "leo wokovu umefika katika nyumba hii". Hidhithi ya Zakayo ni hadhithi yetu pia, kwa sababu Mungu hutafuta yeyote anayepotea na kumrudisha katika neema yake. Lakini kama Zakayo, ni lazima tukubali kwamba tu wenye dhambi na kuungama mbele ya Mungu, ili Kristo atuguze kwa neema yake. Hivyo twahitaji neema ya Mungu ili tuwe wanyenyekevu na kukubali udhaifu wetu wa kibinadamu. Pia twahitaji nguvu za kufungua mioyo yetu, ili tupate kusikia Kristo akituita tushuke chini kama Zakayo, na kumpokea Bwana kwenye nyumba yetu, yaani katika maisha yetu. Kwa kumkaribia Bwana, Zakayo aligeuka kabisa akaamua hata kuwapa masikini nusu ya mali yake, na kuwarudishia wote ambao alikuwa amewadanganya. Basi kuna ujumbe gani tungepeleka nyumbani Jumapili hii? 1) Hadithi ya Zakayo yatusaidia kuelewa na fumbo la Mungu mwenye huruma anayewatafuta na kuwaokoa wenye dhambi; 2) Kama vile Zakayo alivutwa na tamaa ya kumwona Yesu, hata leo Mungu huenda akatumia ujasusi wa watu kuhusu Kanina Katoliki ili kuwakaribisha karibu na Yesu awaguze; 3) Kama Zakayo hata sisi pia lazima tuyahatarishe maisha yetu na jina letu ili tuguzwe na neema la Mungu katika Kristo, anayetuokoa; 4) Hivyo pia, kama wafuasi wa Kristo, lazima tuwe na uhodari kama Yesu mwenyewe, ili kuwaongoza wenzetu kwa Kristo.

©2010 John S. Mbinda

No comments: