Friday, January 1, 2010

3 Januari Sherehe za Epifania la Bwana Mwaka C

3 Januari Sherehe za Epifania la Bwana Mwaka C
Insha: Kristo Amefunuliwa kwa Watu Wote
Masomo: Isaya 60:1-6; Waefeso 3:2-3, 5-6; Matayo 2:1-12

Jumapili hii tunaadhimisha siku kuu ya Epifania ambae pia yajulikana kama Krisimasi ndogo. Epifania maana yake ni “onyesho” – yaani kuonyeshwa na kufunuliwa wazi kwa Kristo kwa mataifa yote duniani. Epinania yatukumbusha fumbo la Kristo, aliye mtoto na pia mfalme. Kwa siku kuu hii, Kristo hufunuliwa kwa watu wote duniani kama Mkombozi. Kwenye utangulizi wa Kanuni ya Misa ya Epifania, twaelezwa umaana wa fumbo tunayoadhimisha. “Kwa maana katika Kristo umefunua leo fumbo la wokovu wetu liwaangazie mataifa”. Mtk. Paulo kwenye Somo la Pili anatuambia, “Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; …ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa uruthi mmoja na mwili mmoja na washiriki pamoja nasi… kwa njia ya Injili”. Kwa maneno mengine tunafundishwa kwamba Mungu uwakomboa watu wote bila kubagua. Mtk. Paulo basi anatufundisha kwamba ahadi ya Mkombozi Yesu Kristo haikuwa kwa ajili ya Mayahudi tu, bali ni kwa mataifa yote. Basi tunapotoa ushuhuda wa ukombozi, tufanye hivyo kama vile Mungu angefanya, bila ubaguzi au ukabila.

Masomo ya Siku kuu hii yatualika twende pamoja na Mama¬jusi, safaniri yao kwenda Bethlehemu, kumwona Mtoto aliyezaliwa kuwa Mwokozi wetu. Pamoja nao tuanguke mbele yake tumsujudie, tumwabudu na tupokee mwanga aliyotuletea mioyoni mwetu. Kwenye siku kuu ya Epifania tunaadhimisha kuonyeshwa wazi na kufunuliwa kwa Mungu katika Kristo maishani ya watu wote. Kama wale Mamajusi kule Bethlehemu, nasi pia tufurahi kwa sababu twamkuta Mtoto Yesu na Maria mamaye pangoni. Epifania hasa yaonyesha wazi wajibu wetu kama Wakristo. Kwa maisha yetu kila siku, wakati tuwapendao wengine, wakati tunapowasamehe, katika imani na huruma yetu, kwenye mfano wetu wa uvumilivu, tutawasaidia wengine kumgundua Kristo mwanga wa kweli. Kuna hadithi ya mwanamke mmoja aliyekuwa na shida na parokia lake. Kwa mda mrefu hakwenda kanisani. Shida lake hasa ilikuwa kwamba hakuelewa na mafundisho juu ya ufufuko wa Bwana. Siku moja mwanamke huyo alikutata na rafiki yake Mkatoliki. Walipoanza mazungumzo kuhusu imani yao, yule mwanamke akasema kwamba yeye hakuamini umaana wa kwenda kanisani. Rafiki yake akashangaa. Basi yule rafiki akaelewa kwamba, labda rafiki yake angefaidika kwenda kumwona padre ili aeleze shida lake. Yula rafiki akampembeleza na mwishowe akakubali kwenda kwa padre. Hapo afisini ya parokia, yule mwanamke aliingiliwa na mang’amuzi ya pekee. Kwa mara ya kwanza, padre alimpokea kwa heshima na ukaribisho. Jinsi yule padre alisikiliza kwa makini hadithi lake la kukaa nje ya kanisa; yale majibu ya paroko yule paroko yaliojazwa na huruma hayo yote yakamfanya yule mwanamke kulia machozi. Ndipo alianza kuona mwanga katika ngiza la safari yake ya imani. Alipoinuka kwenda zake, alimwambia paroko, “leo kweli nimegundua nyota itakayoniongoza hadi nifikie mwanga wa kweli.” Huo ndio ujumbe wa sherehe za Epifania. Kama yule rafiki wa mwanamke kwenye hadithi tuzidi kuishi katika neema ya Epifania, ili tuweze kumfunua Kristo kwa ushuhuda wa maisha yetu kwa wengine mahali tunapoishi, katika familia, shuleni au kazini.

©2009 John S. Mbinda

No comments: