Thursday, December 24, 2009

25 Disemba: Siku kuu ya Kuzaliwa kwa Mwokozi, Krisimasi

25 Disemba: Siku kuu ya Kuzaliwa kwa Mwokozi, Krisimasi
Insha: Msiogope, maana leo amezaliwa Mwokozi
Masomo: (Misa Usiku) Isaya 9:2-7; Tito 2:11-14; Luka 2:1-14

Karibu miaka elfu mbili iliyopita usiku fulani, wakati kulikuwa kimya kabisa kule mji wa Bethlehemu, kulitukia kitu cha ajabu. Mtoto Yesu alizaliwa na Bikira Maria. Ndiyo sababu Wakristo duniani kote wanaadhimisha kwa shangwe kuzaliwa kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo; wakati Mungu alijifunua katika Mwanae, akawa mtu - Mungu pamoja nasi - Imanuaeli. Kwenye Siku kuu hii, tunaadhimisha kwa furaha habari Njema aliyetangaza Malaika akisema: "maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa kwa ajili yenu; Mwokozi, ndiye Kristo Bwana". Basi tuungane na Kanisa popote duniani tuiadhimishe kwa shangwe Siku kuu hii ya Kristo kati yetu, aliyezaliwa na Bikira Maria. Kwa muda wa wiki 4 za Majilio tumejitayarisha kwa ajili ya Sikukuu ya Krisimasi, ambao ni utimilifu wa utabiri wa nabii Isaya kwenye somo la kwanza katika Misa ya Usiku. “Maana kwa ajili yenu mtoto amezaliwa”. Katika sala ya Misa ya Krisimasi, tunaalikwa kumkaribisha Kristo kama Mwokozi wetu; tukeshe tukingojea upambazuko wa ukombozi wetu, wakati Neno wa Mungu alitoka mbinguni, akachukua ubinadamu wetu. Kwa hivyo tufurahi, kwa sababu wokovu tulioahidiwa sasa umetimia; Mwokozi wetu amezaliwa; mwanga wetu umeingia duniani. "Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza".

Wakati huu wa Krisimasi Kristo awe nuru yetu maishani mwetu. Masomo hasa yatujaza furaha kuu na shangao mbele ya fumbo la mtoto aliyezaliwa. Siku kuu ile ya kwanza huko Bethlehemu, nuru iling’ara kwenye ngiza. Kristo alizaliwa na Maria na akalazwa pangoni, “kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni”. Hivyo Yesu alizaliwa katika umasikini, ili Mungu awavutie wachungaji na wote walio masikini. Masomo basi yatualika twende pamoja na Wachungaji "mpaka Bethelehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana". Ujumbe hasa ni kwamba pamoja na Maria na Yosefu tutafakari kuhusu fumbo la Mungu kati yetu. Tumtukuze na kumshukuru kwa ajili ya wokovu wetu katika Kristo. Namtakieni heri na fanaka za Krisimasi, ili Mwenyezi Mungu amjaze na upendo wake, amani na furaha kuu wakati huu wa Krisimasi na katika Mwaka Mpya ujao.

©2009 John S. Mbinda

No comments: