Thursday, April 10, 2014

Jumapili ya Matawi Mwaka A

Jumapili ya Matawi Mwaka AInsha: Mbarikiwa Ajaye kwa Jina la BwanaMasomo: Is 50:4-7; Waf 2:6-11; Mat 26:14-27

Kwa sherehe za Jumapili hii ya Matawi, Kanisa huadhimisha ukubusho wa Bwana Yesu wakati aliingia Yerusalemu mahali atakapokamilisha fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kufa na kufufuka kwake. Jumapili ya Mateso ina pande mbili: Kwanza tunabariki matawi huko mlangoni mwa Kanisa, halafu hufuata maandamano. Kwa maandamano ya matawi Jumapili hii, tunaanza rasmi Wiki Takatifu tukielekea Pasaka la Bwana. Maandamano yenyewe humshangilia Yesu, ambaye hivi punde wale waliomshangilia ni wale wale watakaomtolea asulubiwe bila kosa lolote.  Kwa kifo na ufufuko wake, Yesu Kristo atarudi kwenye utukufu wa Baba. Hivyo Jumapili ya Matawi ina pande mbili, yaani pande moja ya furaha, mashangilio na ishara za utukufu; na pande nyingine ya mateso na kifo msalabani. Tunaona kwanza Yesu akiingia Yerusalemu kwa shangwe na furaha, na pia kuna mateso yatakayompata hivi punde. Yule anayeingia Yerusalemu kwa shangwe, ndiye pia atayehukumiwa na umati afe msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Kama vile tunavyosikia kutoka Mtk. Paulo kwenye Somo la Pili, Yesu, “ingawa alikuwa sawa na Mungu, hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikamana nacho, bali alijifanya si kitu, akajifanya sawa na mtumwa, akazaliwa katika umbo la mwanadamu. Naye akiwa na umbo la mwanadamu, alijinyenyekeza hata mauti, naam, mauti ya msalaba!” Hivyo Yesu ndiye mfano maalum wa kutuonyesha jinsi safari yetu ya imani hapa duniani itakapokuwa hapo mwishowe, yaani kujinyenyekesha na kuteswa hadi kukubali kufa msalabani, ili Mungu atufufue siku ya mwisho.

Pande ya pili ya Jumapili hii ya Matawi huanza kwa Masomo ambao ni Liturgia rasmi ya leo. Hasa Injili ya Jumapili hii yahusu mateso ya Bwana kama ilivyoandikwa na Mathayo. Kwenye kifungu hiki, Injili yenyewe ni kama mchezo wa kuigiza ambapo kuna wasanii kadhaa, Yesu mwenyewe akichukua yumo mahali pa katikati. Tunapoendea kuzikiliza mateso ya Bwana Jumapili hii, tungejiuliza hivi: je, mimi ningejilinganisha na msanii yupi kwenye mchezo huu? Kuna Yuda Iskarioti aliyemsaliti Yesu; kuna Barabas aliyependelewa na umati aachiliwe badala ya Yesu. Pia kuna makuhani wakuu na waalimu wa sheria waliokuwa wakitafuta njia yeyote ya kumshtaki Yesu; kuna umati uliokuwa ukipendelea na kuchochea Yesu asulubiwe, na hapo baadaye askari wanamtukana Yesu na kumtemea mate wakati anakufa msalabani. Tupende tusipende, sisi zote tungelaumiwa kwa ajili ya dhambi zetu zilizosababisha kuhukumiwa kwa Yesu afe msalabani. Jumapili hii na pia maishani yetu yote, mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo lazima yatugeuze kiroho, ili tujitayarishe kuzifuata nyayo zake, kwa kuachilia mabo yote ya ngiza, na kufanya vile alifanya kwa kuyakubali mateso. Basi wakati huu wa Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo na ufufuko wake yadumishe imani yetu, na kututilia nguvu tuweze kushuhudia ukweli wa imani yetu bila woga. Tumwombe Bwana atusamehe kwa kuwa hasa sisi pia tumemsaliti na kumkana kama Judasi na mtume Petro. Kuna ujumbe gani tungepeleka nyumbani Jumapili hii? 1) Mateso ya Bwana yatugusa kindani sana na hutuongoza kujuta dhambi nzetu, ili tuweze kufuata mfano wa Yesu, ambae alijinyenyekesha, akawa binadamu hadi akafa msalabani ili atukomboe. 2) Jumapili ya Pasaka yatuonyesha njia ya kwenda hadi Ijumaa Kuu na kuelekea Ufufuko wa Bwana. Yatukimbusha kwamba hamna ufufuko bila Ijumaa Kuu, yaani bila kupitia kwenye mateso na kifo cha Bwana, ili nasi tufufuke pamoja naye katika maisha mapya.


©2014 John S. Mbinda

Tuesday, April 1, 2014

Jumapili ya 5 ya Kwaresima Mwaka A

Jumapili ya 5 ya Kwaresima Mwaka A
Insha: Mimi Ndio Ufufuko na Uzima
Masomo: Ezekieli 37:12-14; Warumi 8:8-11; Yohana 11:1-45

Jumapili mbili ziliopita, tulisikia Injili kuhusu yule Mwanamke Msamaria, na kisha Jumapili iliyopita juu ya kuponywa kwa yule mtu kipofu tangu kuzaliwa. Jumapili hii ya Tano ya Kwaresima, masomo yote tatu yatupeleka hatua yingine mbele, ili tumgudue Kristo ambaye sio tu maji ya uzima na nuru ya ulimwengu, mbali pia Yesu ndiye ufufuko na uzima. Kwa masomo haya, na hasa Injili yenyewe, tunaanza kuingi pole pole kwenye mawazo ya fumbo la Pasaka. Masomo yenyewe yatukumbusha hali halisi ya uchungu unaotokana na kifo katika familia. Pia twakumbushwa juu ya msiba wa kifo ulioko mbarani Afrika kila siku kutokana na magonjwa ya haina nyingi, na shida za kila aina, zinazosababisha watu wengi kupoteza matumaini na lengo halisi la maisha; watu ambao wanaonekana kama tayari wamekufa. Lakini Nabii Ezekieli anatuambia kwamba, hata ingawa Afrika huenda ikalinganishwa na lile bonde la mifupa aliyoiona, siku moja Mungu atawapatia wana wa Afrika maisha mapya na nguvu ya kutosha, ili mbara letu liendelee mbele. Basi Nabii Ezekieli anatuambia kwamba kwa wote wanaomwamini Mungu wa uzima, kuna uzima na matumaini. Hivyo tusikate tamaa kamwe.

Sisi zote tumepatwa na msiba kwa ajili ya kifo kwenye familia au kijijini kama vile tunasikia kwenye Injili ya Jumapili hii kuhusu kifo cha Lazaro, na vile Yesu alikuja kumfufua. Lakini tukumbuke kwamba, wakati Yesu alipashwa habari za ugonjwa wa rafiki yake Lararo, Yesu alikawia siku nne, ili kwa mujiza wa kumfufua Lazaro umtukuze Mungu Baba, naye Mwanae pia atukuzwe. Yaani ili mujiza huo uwe kama ufunuo kuhusu Baba na kuhakikisha kwamba ndiye aliyemtuma Mwanae Yesu Kristu. Ule mujiza wa kumfufua Lazaro watukumbusha kwamba Yesu ndiye asili ya uzima; yeye ndiye uzima na ufufuko. Kama vile wakati wa msiba nyumbani watu hupatwa na huzuni na kutoa machozi, pia kwenye Injili hii Martha na Maria bila shaka wamejazwa na machozi wakati wanaomwambia Yesu kwamba ndugu yao hangefariki kama Yesu angekuwa nyumbani mwao. Yesu pia kwa utu wake anatoa machozi. Hatimaye, Yesu anachukua nafasi hiyo kuwaongoza Martha na Maria hadi kujifunua yeye mwenyewe: “Mimi ndimi ufufuko na uzima. Anayeniamini mimi hata kama anakufa ataishi; na kila anayeishi na kuniamini hatakufa kamwe”. Mazungumzo hayo baina ya Yesu na Martha na Maria ni mafundisho ya maana kwa imani yetu kuhusu Yesu anayeweza kugeuza kifo kiwe uhai na msiba kuwa furaha. Ujumbe hasa tunge chukua kotokana na masomo ya Jumapili hii ni mawazo matatu 1) Yesu aliwaongoza Martha na Maria hadi wakadumiza imani kuhusu yeye aliye ufufuko na uzima. 2) Vivyo hivyo nasi pia tudumize imani yetu katika Yesu Kristo aliye uzima na ufufuko wetu, hasa wakati tuingiapo katika msiba. 3) Liturgia ya leo basi, yaadhimisha Mungu wa uzima, ambaye katika Kristo anashinda mauti na kuleta uzima. Hatuna budi basi kutangaza ujumbe huo ambao ni habari njema kwa walio na msiba au wale waliokata tamaa kwa sababu yeyote.


©2014 John S. Mbinda

Saturday, March 29, 2014

Jumapili ya 4 ya Kwaresima

Jumapili ya 4 ya Kwaresima

Dhamira: Kristo Nuru ya Ulimwengu
Masomo: 1 Samueli 16:1, 6-7,10-13; Waefeso 5:8-14; Yohana 9:1-41

Nuru na ngiza, uwezo wa kuona na upofu, hayo ndo maneno yanaotusaidia kuelewa na ujumbe wa Jumapili hii. Maso mo ya Jumapili hii yatufundisha kwamba Kristo ndiye Nuru ya ulimwengu. Shangilio kabla ya Injili ni kama kitangulizi cha ujumbe wa Jumapili hii. “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye atakuwa na nuru ya uzima” (Yn. 8:12). Ibada la liturgia nzima ni adhimisho la fumbo la Kristo, nuru ya ulimwengu, nuru iondoaye ngiza ya mioyo yetu, ili tumwone Mungu. Jumapili hii tunaadhimisha Kristo ambaye uponya upofu wetu. Kwenye Somo la Kwanza, Samueli anajaribu, kama kwenye  ngiza, kuchagua mfalme wa Israeli, lakini mwishowe anafaulu kumchagua Daudi kwa msaada wa nuru ya Mungu, ambaye huamua sio kulingana na sura ya uso wa mtu, bali usafi wa moyo. Kwenye Somo la Pili, Mtk. Paulo anatukumbusha kwamba, hapo zamani tulikuwa katika giza, lakini sasa tumekuwa nuru katika Bwana, na hivyo yatubidi tuishi kama watoto wa nuru, na sio kama watoto wa giza. “Kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki, na kweli”.

Injili ya Jumapili hii, yahusu kuponywa kwa yule mtu aliyekuwa amezaliwa kipofu. Kwenye hadithi hii, Yesu anatufundisha kwamba wale wanaomwamini wameponywa upofu wa kiroho. Wasiomwamini watabaki katika upofu wao, na hukumu itawaandama. Tunaona basi baada ya kuponywa na Yesu, yule mtu alipata nuru ya imani iliyomwezesha kutangaza wazi imani yake katika Kristo bila woga. Lakini Mafarisayo, walibaki katika hali ya upofu, na hivyo hawakuweza kumwona Yesu au kuelewa na vitendo vyake. Kama wakati ule wa Yesu, hata leo kunao wengi wanaofuata giza iliyo zaidi kuliko upofu wa macho. Kuana ujumbe gani tungepeleka nyumbani Jumapili jii? 1) Tunafundishwa kwamba kwa Ubatizo wetu Kristo aliponya upofu wetu, na akatupatia nuru ya imani, ili kama yule mtu aliyeponywa naye, nasi pia tumuhubiri Kristo bila woga, hata ingawa tutakabiliwa na upinzani wa wale bado wanaishi katika giza. 2) Kwa kutuponya upofu wetu, Kristo ametupatia neema na nguvu za kitume, na hivyo tusiache uwongo na udanganyifu zififie nuru yetu, kwa sababu Kristo ndiye nuru ya ulimwengu. 3) Kuponywa kwetu kwatusaidia tuishi maisha ya nuru, bila kuificha imani yetu katika Kristo. Tunaitwa tushuhudie ukweli mbele ya uwongo; tuwe kama mnara wa nuru mbele ya upinzani.

©2014 John S. Mbinda


Wednesday, March 19, 2014

Jumapili ya 3 ya Kwaresima Mwaka A

Jumapili ya 3 ya Kwaresima Mwaka A
Insha: Kristo - Maji ya Uzima
Masomo: Kutoka 17:3-7; Warumi 5:1-2, 5-8; Yohane 4:5-42

Kiu na maji ya uzima ndio maneno yanaotusaidie kuelewa na fundisho la masomo ya Jumapili hii. Kiini cha masomo ya Jumapili hii ya Tatu ya Kwaresima hasa kutusaidia kujikagua ili tugudue jinsi tunaoitaji Yesu Kristo, ambaye ndiye maji ya kweli yaliyo hai. Jumapili hii ya Tatu ya Kwaresima ndio Jumapili ya “Ukaguzi wa Kwanza” (Scrutinies) wa Wateule wa Ubatizo, yaani wakati wa kujikagua pamoja nao, ili nasi pia tuone jinsi tunaohitaji yale maji ya uzima, yaani Yesu Kristo maishani mwetu. “Yeyote atakayekunywa maji yale nitakayempa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele”. Masomo yote 3 yatumia mfano wa maji ili kutufundisha fumbo la Yesu Kristo ambaye ndiye maji ya kweli. Kwenye somo la kwanza katika Kitabu cha Kutoka, tunasikia jinsi Wana wa Israeli walipatwa na kiu njwangwani na wakaanza kumlalamikia Mungu wakisema kwamba Mungu aliwatoa kutoka Miszi ili wafarikie huko njangwani. Ndipo basi Mungu akaamuru Musa alipige jiwe na bakora lake, na hapo maji yakatoka ili watu wanywe. Mtk. Paulo analinganisha mfano huu wa maji yakibubujika na maji ya Ubatizo wetu, ambayo Mungu ametumiminia neema yake mioyoni mwetu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Kwenye Injili ya Jumapili hii, Yesu yumo kwenye Kisima cha Yakobo mchana saa sita wakati kunao jua kali, naye anasikia kiu. Punde tu, mwanamke Msamaria anakuja kuja kuchota maji. Kwanza Yesu anagudua kiu cha kiroho cha mwanamke huyu ambaye anasifa ya kuolewa mara tano, na sasa anaishi Bwana mwingine. Kwa sababu Yesu anajua siri na hali ya maisha yake, Yesu mwenyewe ana kiu cha cha kugeuza yule mama kiroho. Mara tu wanapoanza mazungumzo, Yesu anaomba maji anywe. Lakini kiu chake sio tu kile cha kimwili, bali ni kiu cha ukombozi wa roho ya mama huyu. Basi kwenye mazungumzo yao, Yesu anamwongoza pole pole, hadi yeye anagudua kiu chake cha kiroho. Basi ndipo Yesu anamshitua kwa kumwambia siri zake zote za kuolewa na wanaume watano. Ndipo basi akiwa na haya ya maisha yake ya siri, neema ya Mungu ilimwingilia yule mama na akaanza kusema, “Najua ya kuwa yuaja Masiha (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote”. Mwishowe tunasikia Yesu akijifunua kabisa kwa mama yule akimesa, “mimi ninayesema nawe, ndiye”. Kwa maneno hayo, yule mama kwanza anashangaa, halafu anageuka moyo kabisa, akimwamini Yesu, na kutamani yale maji yaletao uzima. Hatimaye, yule mama anaacha mtungi wake hapo, na kwenda kama mfuasi wa Yesu huko kijijini na kutangaza, “Njooni mkaone”. Njooni mkaone yule aliyegeuza maisha yangu kabisa. Ujumbe wa masomo ya Jumapili hii ni mawazo matatu: 1) Kama vile yule mwanamke Msamaria aliongozwa na Yesu hadi akagudua kiu chake cha kiroho, sisi pia twashirikishwa kugundua mahitaji yetu ya kutubu ili tupokee huruma wa Mungu. 2) Masomo yatuongo kujikagua, ili tugudue jinsi tunaohitaji yale maji ya uzima, yaani Yesu Krito maishani mwetu 3) Kama vile yule mwanamke Msamaria aligeuka na akawa mfuasi wa Yesu huko kijijini mwake, nasi pia tunaitwa tuingie kwenye maisha mapya ya Yesu, ili wengine wamwamini Yesu kwa ajili ya ushahidi wetu; Yesu aliyegeuza maisha yetu.


©2014 John S. Mbinda

Friday, March 14, 2014

Jumapili ya Pili ya Kwaresima

Jumapili ya Pili ya Kwaresima

Dhamira: Ukristo Wetu ni kama Safari ya Imani
Masomo: Mwanzo 2:1-4; 2 Tim. 1:8-10; Mathayo 17:1-9

"Toka wewe katika nchi yako na jamaa zako, uende mpaka inchi nitakoyokuonyesha". Maneno hayo kutoka Somo la kwanza la Jumapili ya Pili ya Kwaresima, yatupatia kiini cha ujumbe wa Jumapili hii, yaani kama Wakristo tunaitwa tuache nchi yetu na utamaduni wetu na tutoke tuingie safarini ya imani kuelekea mahali Bwana atakapotuonyesha. Huo pia ulikuwa wito wa Mungu kwa Abrahamu. Kwa kawaida sisi wanadamu hupendelea kukaa mahali tulipo na kuwa starehe. Lakini kama Abrahamu, Mungu anatuita tutoke katika nchi yetu twende mahali atakapotuonyesha. Hivyo Ukristo wetu ni kama maisha ya safari ya imani na matumaini katika Mungu. Nchi ya Abrahamu wakati ule kabla ya kuitwa ilikuwa nchi yenye uchumi wa hali ya juu. Lakini dini yao ilikuwa ya kuabudu miungu ya kuwaongeza watu nguvu za kimwili. Hivyo ibada yao ilifanyika mahali paliokuwa na mtindo wa kufanya umayala wa kiume na wa kike. Pia ibada yao ilikuwa kuwatoa watoto wachanga kama sadaka, kwa sababu miungu yao ilidai damu ya watoto.  Basi twaweza kuelewa sababu ya Mungu kumwita Abrahamu aondoke kutoka mazingira ya haina hiyo. Nasi pia twaitwa tuondoke tutoke kwenye vitendo vibofu vya utamaduni wetu tuingie mahali pa neema ya Mungu. Twakumbushwa kwamba, hata ingawa huenda tukapata shida na majaribio njiani, hapo mwisho tutapata ule utukufu tulioahidiwa. Ndiyo sababu Mtk. Paulo anatukumbusha kwamba kwenye safari yetu ya imani tunaelekea mahali tusiopajua, na hivyo tuwe tayari kukabiliwa na shida na mateso. Wakati huu wa Kwaresima, tunaitwa tuvumilie mabaya kwa ajili ya Injili, kwa kadiri  ya nguvu ya Mungu.

Injili ya Jumapili hii ni juu ya Yesu akigeuka sura huko mlimani na umaana wa kitendo hicho maishani mwetu. Mara kwa mara, sisi wanadamu hujaribiwa kuepuka shida zinazoambatana na wito wetu wa Kikristo. Badala ya kuzikabili twapendelea kuziepuka, ili tuwe na utulivu. Kama Mtk. Petro kwenye Injili, mara kwa mara tunaoja utukufu wa Mungu; wakati ambao tungetaka kujenga hema ili tukae starehe katika hali hiyo ya furaha; maisha ambayo hayana shida hata kidogo. Nyakati kama hizi hupita haraka, kama vile kugeuka sura kwa Yesu mlimani kuliwa kwa mda tu, na punde Mitume wakajikuta tena katika hali ya kawaida. Basi nasi pia tuwe tayari siku zote kukabiliwa na shida na majaribio kwenye safari yetu ya imani hapa duniani. Nyakati kama hizo, tukumbuke kwamba hapo mwisho taji ya utukufu yatungojea. Wale wanaomwamini Mungu na kumtumaini daima, siku moja hata wao watageuzwa sura na kuingia katika maisha ya milele mbinguni. Ujumbe wa masomo ya Jumapili hii hasa ni mambo matatu. 1) Tunaitwa tuache usalama wetu na utamaduni wetu tukimtumainia Bwana, ili atugeuze tuishi maisha mapya katika Kristo; 2) Katika dunia ya leo hasa sio sahisi kuishi ukristo wetu kwa sababu huenda marafiki wetu wakatuchekelea hasa tukiishi kulingana na amri za Mungu au za Kanisa, lakini tunaweza kwa neema ya Mungu; 3) Kwa sababu Yesu atupatia nguvu zake, tunaweza pia kuvumilia kuchukua msalaba wetu na kumfuata wakati huu wa Kwaresima, ili tuadhimishe vyema Pasaka la Bwana.


©2014 John M. Mbinda

Friday, March 7, 2014

Jumapili ya Kwanza ya Kwaresima Mwaka A

Jumapili ya Kwanza ya Kwaresima Mwaka A

Insha: Uaminifu katika Neno la Mungu
Masomo: Mwa 2:7-9, 3:1-7; War 5:12-19; Mat 4:1-11

Kiini cha ujumbe wa masomo ya Jumapili ya Kwanza ya Kwaresima chapatikana hasa kwenye maneno matatu, yaani uaminifu, jaribio, na chaguo. Kwenye Somo la kwanza kutoka Kitabu cha Mwanzo, tunasikia ile hadithi kuhusu majaribio na kuanguka kwa wazazi wetu wa kwanza Adamu na Hawa huko shambani la Edeni. Wangechagua kumtii Mungu, lakini wakaamua kuivunja amri yake. Wangechagua kuepuka kishawishi cha kula lile tunda walioamriwa wasile, lakini wakaamua kulichukua na kula. Hivyo wakamkosea Mungu Muumbaji. Wazazi wetu wa kwanza walikuwa wamedanganywa kwamba, wakila uzao wa tunda hilo watapata hekima ya hali ya juu, ili waweze kufanya chochote wapendao bila msaanda wa Mungu. Lakini kwa kweli walijitenga na Mungu, na wakachukua hali ya ugeni, huko wakianza kumwogopa Mungu Muumbaji wao. Kitendo chao kiliwaingiza binadamu wote katika hali ya Dhambi ya Asili. Kutoka kwa wazazi wetu wa kwanza basi tunabeba mbegu za kutotii, kuvunja amri za Mungu na kuwa wenye kujipenda, na hivyo kumkataa Mungu Muumba wetu. Hata hivyo, kwa sababu Mungu ni mwenye rehema, yeye ututafuta ili tutoke kwenye hali ya udhaifu wetu na kutupatanisha naye.

Kwenye Somo la Pili, Mtk. Paulo anatuambia, “Na kama vile watu wengi wamekuwa wenye dhambi kutokana na kutotii kwa mtu mmoja, vivyo hivyo wengi watafanywa kuwa wenye uhusiano mwema na Mungu kutokana na kutii kwa mtu mmoja”. Katika Kristo, yule Adamu wa kale amepoteza utawala wake wa kutotii ambao huongoza binadamu kwenye mauti. Kwa kifo na ufufuko wake, Kristo ndiye Adamu mpya, aondoaye utengamano baina ya binadamu na Mungu. Hivyo Kristo amerudisha uhusiano wa kweli baina yetu na Mungu. Injili ya Jumapili hii hasa yatusaidia kutafakari juu ya mfano wa uaminifu wa Yesu, ambaye ulimwezesha kushinda Shetani. Yesu alijaribiwa kule njangwani, lakini akampinga Shetani, hasa kwa sababu alikuwa mwaninifu kwa Neno la Mungu. Twakumbuka vile Shetani alimjaribu Yesu amwabudu, naye Yesu akamjibu, “nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake”. Haitoshi kuifahamu Neno la Mungu au Amri zake. Nilazima pia tuzifuate kwa uaminifu. Ujumbe wa Jumapili hii hasa ni pointi mbili. 1) Kuna tofauti kubwa baina ya Yesu kwenye Injili ya leo na wazazi wetu wa kwanza kwenye Somo la Kwanza. Waliposhawishiwa na shetani, Adamu na Hawa walidanganyika wakala lile tunda, lakini wakati Yesu alishawishiwa na shetani alifaulu kumshinda. 2) Kama vile Yesu alimshinda shetani nguvu kwa uaminifu wake kwa Baba, nasi pia tunaitwa tuwe waaminifu kwa Neno la Mungu, ili tuweze kushida majaribio ya Shetani wakati huu wa Kwaresima.

©2014 John S. Mbinda


Monday, February 24, 2014

Jumapili ya Nane ya Mwaka A

Jumapili ya Nane ya Mwaka A
Masomo: Is 49:14-15; 1 Kor 4:1-5; Mat 6:24-34

Jumapili hii, masomo yatusaidia kuelewa jinsi Mungu anatujali na kukamilisha mahitaji ya viumbe vyote. Tunafundishwa kumtumainia Mungu wakati wote, lakini tukiangalia ulimwengu wetu, watu wengi hawana matumaini kamwe. Ungefikiria wakati Fulani ambao wewe ulikuwa na mashaka ukifikiria kwamba Mungu yu mbali sana wakati una shida nyingi. Ndiyo sababu nabii Isaya anatukumbusha maneno ya Sayuni (yaani Israeli) akiuliza, “Bwana ameniacha, Bwana amenisahau.” Hiyo ilikuwa ishara ya ukosefu wa matumaini. Kwenye ulimwengu wetu, tunaona dalili za ukosefu wa matumaini maishani, kwa mfano mara kwa mara kwenye jiji zetu Afrika, tunasikia kwamba mama ameacha mtoto wake nje ya mlango wa kanisa. Sababu ni kwamba, mama hule amefikia mwisho, kwani hawezi kumlea mtoto. Lakini nabii Isaya anaakikisha Israeli kwamba Mungu awezi kuwasahau. “Je, mama aweza kumsahau mtoto aliyeko matitini mwake akinyonya? Wala asiwe na huruma juu ya mtoto aliyemzaa? Ingawa anaweza kusahau, Mimi sitakusahau wewe!” Basi kama tusikiavyo, Bwana hawezi kutuacha kamwe. Ndiyo sababu Mtk. Paulo kwenye somo la pili anawafundisha Wakristo wa Korintho wasikate tama, mbali wawe na matumaini, kwa sababu Mungu kwa upendo wake anawajani. Basi kwa sababu Mungu anatuahidi, hata kukifanyikaje, tusipoteze matumaini kamwe. Saburi 62 yatusaidia kutafakari zaidi mafundisho hayo. “Hata wengine wakituacha peke, Mungu yu karibu nasi. Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika kamwe.”

Kwenye Injili ya Jumapili hii, Yesu anaendelea na mafundisho hayo juu ya uaminifu na utengemeo wetu kwa Mungu. Anatumia mifano ili kuwafundisha wafuasi wake kwamba Mungu anajali viumbe vyake vyote. “Waangalieni ndege wa angani, wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? … Nanyi kwa nini kujitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata mfalme Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa kama mojawapo ya hayo maua.” Hivyo kwa sababu Mungu anawajali wanyama na mimea, si atafanya zaidi kwetu sisi binadamu? Basi tumwaminie na kumtumainia Mungu na yote mengine atatujalia. Watakatifu wengi walifuata mafundisho hayo ya Yesu, yaani kuachia yote mikononi mwa Mungu. Walimtegemea Mungu peke kwa mahitaji yao yote. Mfano mmoja ni mtakatifu Francisco wa Assisi. Alikuwa mtoto wa mtu mmoja tajiri sana huko Assisi. Alipoanza safari yake ya kumgeukia Bwana, Francisco alikwenda humo kanisani ya Mtakatifu Damiano na akaikuta imearibika. Ndipo alisikia sauti ya Bwana akisema “Nijengee kanina langu upya.” Ndipo alikwenda kwa baba yake akamwomba urithi wake ili aende kulijenga ile kanisa. Alipoondoka babaye akasikia kwamba Francisco alikuwa na shabaha la kutumia ile pesa kulijenga kanisa. Basi akatuma mfanyi kazi kumwita Francisco. Aliporudi, akakuta babaye na umati wa jiji lote pamoja na Askofu wa jimbo. Ndipo babaye akamwambia Frasncisco arudishe pesa yote. Aliporudisha ile pesa, Francisco akasema, “na hata nguo hizi ninazovaa ni zako, zichukue pia.” Hapo Francisco akatoa nguo zote akaachwa uchi! Askofu kwa huruma akatoa kabuti lake akamvyeka. Siku ile, kwa ile ishara ya kuwa uchi, Francisco alimgeukia Bwana kabisa na kutegemea. Ndipo akaanza kuhubiri fafundisho ya umasikini mbele ya Bwana, na vijana wengi wakafuata mfano wake. Sisi zote tunaitwa pia kuacha yote mikononi mwa Bwana. Ndiyo sababu Yesu anatufundisha tafute kwanza ufalme wa Mungu na mengine yote tutayapata. Kwa hiyo tusiwe na wasi wasi kuhusu kesho, yaani tukiwa na masumbuko, kwa sababu Mungu anatujanli. Hiyo sio kusema kwamba hatufanyi kazi, ila ni kutufundisha tusiache masumbuko ya dunia hii yatutawale. Kuwa Mkristo ni kuweka Mungu kwanza mbele ya shughuli zetu zote. Kuna ujumbe gani tungepeleka nyumbani Jumapili hii? 1) Kwa sababu Mungu anawajali wanyama na mimea, hivyo pia atawajali binadamu hata zaidi. 2) Masomo basi yanatufundisha tumwaminie na kumtumainia Mungu na yote mengine atatujalia. 3) Pia tunaitwa kuwawiga watakatifu waliosikiliza wito huo wa Yesu kuacha yote na kumfuata, tukitafuta kwanza ufalme wa Mungu, ili mengine yote tuongezewe.


©2014 John S. Mbinda